Wednesday, 18 October 2017

DAMU YA YESU INAVYOWEZA KUKUTOA ULIPOKWAMISHWA NA URITHI MBAYA

SEMINA YA NENO LA MUNGU UWANJA WA TANGANYIKA PACKERS - DAR ES SALAAM

MWL.CHRISTOPHER MWAKASEGE

TAREHE 15 OKTOBA 2017

*SIKU YA NANE*
*👉NAMBA ZA SADAKA*
http://www.mwakasege.org/kuchangia.htm
*👉KUSIKILIZA MAOMBI PALE MWISHONI BONYEZA MAANDISHI HAYA* https://drive.google.com/…/0B3OfNJtOXYXuLWdEYW9GLXV3a…/view…
*👉LINK YA SEMINA YA LEO YOUTUBE*. SUBSCRIBE Youtube channel ya Mwalimu Christopher Mwakasege uweze kupata updates na alert za semina na masomo mapya
https://youtu.be/b1RAlWUOYhc
*👉KUPATA CD & DVDs ZA SOMO HILI.*
Hii ni summary ya siku ya nane ya somo hili hapa Dar es Salaam. Tembelea www.mwakasege.org kupata maelezo zaidi na kununua Kanda, CDs ama DVDs za siku zote kuanzia siku ya kwanza ili uweze kupata undani wa somo hili. Cd za semina hii zinapatikana *Luther house ghorofa ya tatu karibu na kanisa la KKKT AZANIA FRONT POSTA ( DAR ES SALAAM) au wasiliana na Dina 0754766517*
*Note: Pia unaweza ukasoma vizuri zaidi kwa google plus, Copy hili somo na paste na post google+ kwenye account yako utasoma vizuri na utaona bold na italic kama huoni hapa whatsapp*
*LENGO LA SOMO*.
_*Kuweza kutumia DAMU YA YESU ili uweze kujitoa katika urithi mbaya.*_
Leo nataka tuangalie
*FAIDA ZA KUIMARISHA IMANI YAKO BINAFSI KIMATENDO JUU YA DAMU YA YESU*
Ili iweze kukusaidia kushughulika na urithi mbaya unaokwamisha maisha yake.
*WARUMI 3:23-26*
_“Kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu; wanahesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu; ambaye Mungu amekwisha kumweka awe upatanisho kwa njia ya imani katika damu yake, ili aonyeshe haki yake, kwa sababu ya kuziachilia katika ustahimili wa Mungu dhambi zote zilizotangulia kufanywa; apate kuonyesha haki yake wakati huu, ili awe mwenye haki na mwenye kumhesabu haki yeye amwaminiye Yesu.”_
Nataka uone neno kwa imani katika DAMU yake. Tafsiri ya neno *njia* kibiblia maana yake ni _*mkakati yaani strategy.*_ Kwa hiyo anaposema mawazo yangu si mawazo yenu au njia zangu si njia zenu anataka kutuambia juu ya mkakati wa kukufikisha mahali. Hazungumzii tu njia kama ya kupita.
Kwa hiyo MUNGU anaposema njia itazame kwa jicho pana kidogo, kwa hiyo unaposikia jinsi gani kijana aisafishe njia [mkakati] yake ni kwa kutii na kwa kufuata neno la MUNGU.
Kwa hiyo maandiko yanaposema “kwa njia ya imani katika damu yake, angalia kwa upana kidogo au nenda na tafsiri hii *“kuna njia ya au mkakati wa imani katika DAMU YA YESU”*, kama kuna kwa njia inamaanisha kuna njia.
Kwa hiyo tazama kuna njia ya imani katika DAMU YA YESU unayotakiwa kuitumia. Kwa hiyo unaweza ondoa neno *njia* na ukaweka *mkakati* sababu kama ni kwa mkakati ina maanisha kuna mkakati. Hivyo itasomeka hivi _“kwa mkakati wa imani katika damu yake”_
Kwa hiyo kama unaenda vizuri kidarasa unatafuta kujua kwanza huo mkakati kabla ya kutembea kwanza kwenye huo mkakati.
Maandiko yanasema NENO ni Nuru, na taa miguu pangu. MUNGU hakuongozi tu kwenye njia bali anakuongoza na hatua zako, kwa hiyo huwezi sema unatembea tu kwenye njia bila hatua,maana hatu aza mwenye haki zinaongozwa na BWANA. Biblia inasema neno lake ni taa na nuru miguuni petu yaani ni mwanga wa njia, maana yake inakulazimu kutazama vizuri mkakati.
Kama uko jeshini au kama unatazama sinema za vita, yaani utajua kuwa hakuna kiongozi anaruhusu watu wake kutumia mkakati wasio ujua kabla, kwa hiyo wale viongozi wa kikundi vidogo vidogo na mkakati ulioko, sasa afande anaona mkakati sasa wewe unaweza ukawa unatazama sehemu yako tu lakini kiongozi anaona Askari wa kawaida, askari wa mizinga, hawa wa ndege n.k Wote anawatazama kwa pamoja, wewe ni askari wa mguu unataka kujitazama kivyako ila haiendi namna hiyo. unaweza ukasema Damu ya Yesu ni silaha na unapozungumzia, silaha ina maana unataja vita yaani uwanja wa mapambano kwa hiyo lazima utazame katika upana wake.
Sasa maandiko yanasema “kwa njia ya imani katika damu yake, ili aonyeshe haki yake, kwa sababu ya kuziachilia katika ustahimili wa *Mungu dhambi zote zilizotangulia kufanywa*; *apate kuonyesha haki yake wakati huu*,[sasa hapa ni dhambi zilitangulia kufanywa na zinaleta shida wakati huu]. ili awe mwenye haki na mwenye kumhesabu haki yeye amwaminiye Yesu”. Kwa hiyo anataka mkakati wa Damu yake ufanye kazi ili aoneshe haki yake kwamba anaweza akashughulikia dhambi zilizotangulia kufanywa ili aoneshe haki yake wakati huu.
Sasa ukisoma *Yakobo 2:20*
_Lakini wataka kujua, wewe mwanadamu usiye kitu, kwamba imani pasipo matendo haizai?_ [maana yake imani inatakiwa izae na ili iweze kuzaa inahitaji uhai].
*Yakobo 2:26* inatupa kujua kuwa Imani pasipo matendo imekufa, kwa hiyo ukitaka kupima imani pima matokeo sio mistari jinsi ilivyo. Imani inaletwa kwako ili izae na sio pambo kama yalivyo mapambo mengine. Imani inatakiwa ikuletee matokeo yaliyofanya imani yako. maana *Warumi 10:17* inasema _“Basi imani chanzo chake ni kusikia na kusikia huja kwa neno la Kristo”_ kwa hiyo hilo neno lililokufanya ukasikia linatakiwa likupe matokeo.
Sasa kama imani yako iko hai inafanya kazi tutaangalia matokeo yaani matunda maana mistari uliyoshika haikusaidii.
Sasa sikuambii kuwa na mistari mingi ya biblia ni vibaya niulize mimi nitakusimulia, najitahidi kusoma biblia kila mwaka na nimalize na ili nisichoke kila mwaka nanunua biblia Mpya, kwa hiyo nasoma mwanzo mpaka ufunuo, kwa sababu kusikia huja kwa neno la Kristo. Kwa hiyo kama nimesoma 20% ya biblia ina maana nitasikia kwa 20% kitu Mungu anasema, ksa hiyo ili kusikia zaidi inabid niongeze kusoma neno la Mungu.
Maana kusikia hakuji kwa kuomba, bali huja kwa kusikia neno, kwa hiyo kama huna neno unaweza msikia Mungu akisema ila usisikie anachosema.
Ndivyo biblia inasema unaweza ukasikia, na usielewe kwa hiyo kama nataka kumsikia kwa wigo mpana Mungu inatakiwa nijaze neno la Bwana ndani na sio nijaze tu neno bali, nilisaidie kile ambacho Mungu anataka nipate, na ndani yake inatengeneza imani.
Kwa hiyo ninapoona eneo fulani ndani yangu halina matokeo ya kibiblia, kwa lugha nyepesi ni kuwa imani uliyonayo imekufa. Usijaribu kujihesabia haki, imani yako haina matendo, shetani nae imani anayo kwa hiyo msitishane. Kwa hiyo ninachosikia rohoni, ni kwamba uweze kuimarisha imani yako kimatendo juu ya DAMU YA YESU wewe mwenyewe.
Nilipoamka leo nilikaa na nikamweleza mke wangu na nikamwambia kuwa leo ni siku ya ajabu sana akaniuliza kwanini nilimwambia ni kama hii semina iliisha jana, akaniuliza kwanini nikamwambia leo sina kitu cha kusema maana Mungu hajanipa cha kusema kwa sababu kuna semina naweza ona mapema, mfano naweza jua kuwa semina ya mbeya itakuwa nini kwa siku tatu au nikajua semina ya mwaka ujao.
Sasa ya leo sikuona kitu, kwa hiyo mke wangu akasema huenda tumeongeza siku ambazo Mungu hakutaka tuweke nikasema semina ya leo iko ila sijui Kwanini Mungu kanyamaza, na nikasema redio yangu huku ndani iko wazi, akisema saa hiyo hiyo nitasikia. Basi baada ya masaa mawili Mungu alinisemesha na kasisitiza hiki ninachokuambia. *kuwa na imani binafsi ya kimatendo juu ya Damu ya Yesu*.
*Waebrania 11:28*
_Kwa imani akaifanya Pasaka, na kule kunyunyiza damu, ili yule mwenye kuwaangamiza wazaliwa wa kwanza asiwaguse wao._
*1 Wakorintho 5:7*
_Basi, jisafisheni, mkatoe ile chachu ya kale, mpate kuwa donge jipya, kama vile mlivyo hamkutiwa chachu. Kwa maana Pasaka wetu amekwisha kutolewa kuwa sadaka, yaani, Kristo;_
Kwa hiyo agano la kale walikuwa na Pasaka na agano jipya tuna pasaka. Kwa hiyo hakukuwa na haja ya pasaka leo kama kusingekuwa na unahitaji wa Pasaka wakati huu kama kusingekuwa na tatizo linalohitaji msaada wa mkakati huu, wa Damu ya sadaka iliyoitwa Pasaka.
Tofauti yake ni kwamba matatizo ni yale yale na mkakati ni ule ule, ila kinachotumika ndani kiko tofauti, walitumia damu ya kondoo ila sasa tunatumia damu ya Yesu.
Kwa hiyo huwezi soma huo mstari wa *1 Wakoritho 5:7* bila kurudi na kutafuta yule Pasaka wa kwanza namna alivyotolewa kwa imani.
Ngoja nikupe faida kadhaa hapa, kama nne hivi ambazo zitakusaidia kupata shauku ili ujenge imani yako kimatendo kutoka katika habari hii ya Musa.
*1. IMANI YAKO HIYO ITAKUSAIDIA IKIWA MUSA WAKO HATAPEWA MAELEZO YA KUPEWA KUTUMIA DAMU YA YESU KWA NIABA YAKO*.
Ukisoma *Waebrania 11:28* bila kuangalia ilipotoka utafikiri Musa alichinja pasaka kwa niaba ya wengine wote angalia _“Kwa imani akaifanya Pasaka, *na kule kunyunyiza damu*, ili yule mwenye kuwaangamiza wazaliwa wa kwanza asiwaguse wao”._
Ilivyoandikwa unaweza ukafikiri Musa alitoa kwa niaba yao, ila haiko hivyo angalia;
*Kutoka 12:1-4,7*
_BWANA akanena na Musa na Haruni katika nchi ya Misri, akawaambia, Mwezi huu utakuwa mwanzo wa miezi kwenu; utakuwa ni mwezi wa kwanza wa mwaka kwenu. Semeni na mkutano wote wa Israeli, mkawaambie, Siku ya kumi ya mwezi huu kila mtu atatwaa mwana-kondoo, kwa hesabu ya nyumba ya baba zao, mwana-kondoo kwa watu wa nyumba moja; na ikiwa watu wa nyumba ni wachache kwa mwana-kondoo, basi yeye na jirani yake aliye karibu na nyumba yake na watwae mwana-kondoo mmoja, kwa kadiri ya hesabu ya watu; kwa kadiri ya ulaji wa kila mtu, ndivyo mtakavyofanya hesabu yenu kwa yule mwana-kondoo. *Nao watatwaa baadhi ya damu yake na kuitia katika miimo miwili na katika kizingiti cha juu, katika zile nyumba watakazomla.*_
Angalia vizuri ule mstari wa tatu _“Semeni na mkutano wote wa Israeli, mkawaambie, Siku ya kumi ya mwezi *huu kila mtu atatwaa mwana-kondoo*, kwa hesabu ya nyumba ya baba zao, mwana-kondoo kwa watu wa nyumba moja”_
Kwa hiyo kama mko watano, ina maana mwana kondoo mmoja, kwanini alisema kila mtu, kwa tafsiri ya kawaida kila mtu maana yake aende kwenye zizi na achukue kondoo wake. Kwa hiyo baba achukue mama achukue na mtoto achukue.
Lakini ukisoma biblia vizuri inasema mwanakondoo mmoja na watu walioko kule ndani. Lakini alipokuwa anasema kila mmoja maana yake nini?
Mungu alikuwa anazungumza nao kuwaonesha umuhimu wa kuwa na imani binafsi kila mmoja, kwa hiyo haijalishi ni nani anaenda kuchukua mwana kondoo kiimani kila mmoja ndani ya familia ahusike kwenda kuchukua mwana kondoo.
Biblia inazungumza mstari wa saba juu ya application yake anasema _*“Nao watatwaa [sasa kama mko saba ndani ya nyumba mtatwaa ile damu na kupaka kwenye miimo ya milango na kizingiti cha juu kila mmoja lazima ashiriki], baadhi ya damu yake na kuitia katika miimo miwili na katika kizingiti cha juu, katika zile nyumba watakazomla.”*_
Kwa *hiyo kama* kumi ina maana mtashikilia kila mmoja kupaka hapo. Huyu ni Mungu anazungumza na Musa na alisema kila mmoja atatwaa. Sasa angeweza kusema kiongozi wao ndio atwae. Lakini alipokuwa anaweka watu wote wahusikie alikuwa anazungumza juu ya imani yao maana wasomaji wa Biblia wanajua kabisa, imani ni mkono ina maana unapomsindikiza mwenzako kwa imani ina maana unaenda pamoja nae, alipo upo, anachofanya na wewe unafanya.
Kwanini nimekueleza jambo hili kwa sababu huoni Mungu akimuambia Musa nenda kachukue kondoo alafu chinja kwa ajili ya kila nyumba, huoni maelekezo hayo. Na inahitaji nidhamu sana kwa mtumishi kuweza kuwaeleza mambo hayo kwa sababu wameona namna Farao alivyosumbua na hawakuona usumbufu wake kwa sababu Musa na Haruni ndio walimuona Mungu wakiwa wawili hawa wengine wako nyumbani kwao wanaendelea na shughuli zingine. Yeye peke yake ndio alikuwa anapambana na Farao na kushughulika na Mungu.
Sasa inapofika katika lile pigo la Mwisho, Haruhusiwi kufanya kwa niaba yao anataka kila mtu, sasa wewe fikiri ndio unataka akufanyie. Unaweza shangaa unamkuta Musa wa kwako ili akusaidie na anakuambia Mungu hakunipa maelekezo. Sasa unahitaji nidhamu kali ya kumtii Mungu kuliko kufuata cha watu.
Hapo watumishi wengi sana tunakwama, kwa sababu tunawaogopa watu kwa hiyo tunafanya vitu vingine ambavyo Mungu hakusema. Kama Musa wako hakupewa maelezo ya kutumia Damu kwa niaba yako, saa nyingine Musa wako atapewa, *saa nyingine kama hajapewa nani atakusaidia kama huna imani yako binafsi?.*
*2. IMANI YAKO BINAFSI ITAKUSAIDIA WAKATI MUSA WAKO AMEKOSA NAFASI YA KUKUSAIDIA WAKATI AKIWA NA MAJUKUMU MENGINE WAKATI UNAMHITAJI*
*Kutoka 12:21-23*
_Hapo ndipo Musa akawaita wazee wa Israeli, na kuwaambia, Nendeni, mkajitwalie wana-kondoo kama jamaa zenu zilivyo mkamchinje pasaka. Nanyi twaeni tawi la hisopu, mkalichovye katika ile damu iliyo bakulini na kukipiga kizingiti cha juu, na miimo miwili ya mlango, kwa hiyo damu iliyo katika bakuli; tena mtu ye yote miongoni mwenu asitoke mlangoni mwa nyumba yake hata asubuhi. Kwa kuwa BWANA atapita ili awapige hao Wamisri; na hapo atakapoiona hiyo damu katika kizingiti cha juu, na katika ile miimo miwili, BWANA atapita juu ya mlango, wala hatamwacha mwenye kuharibu aingie nyumbani mwenu kuwapiga ninyi._
Musa alisema maneno magumu kidogo kuwa kila nyumba wakipaka damu hawaruhusiwi kutoka kama wanataka msaada, ile damu ilikuwa inashughulika na kitu gani? *Warumi 3: 23-25* ule wa 23 unasema _“wote wametenda dhambi na kupungukiwa na utukufu wa Mungu. Pia anazungumza juu ya Damu na pia anazungumza juu ya imani.”_
Kwa hiyo kuna dhambi zilizotangulia kufanywa zinazowakwamisha watu katika maisha yao. Wana wa Israel katika kipindi kile cha Musa, walikuwa wanashughulika na urithi mbaya uliotokana na watoto wa Mzee Yakobo. Yakobo hakuwa na shida kwa watoto wake ila watoto wake ndio walileta shida walipomuuza mwenzao.
Mungu alimwambia Ibrahimu, kuwa watoto wako watakuwa watumwa katika nchi isiyokuwa yao. Na tunajua kuwa walienda Misri kwa sababu ya njaa. Sasa hawa wengine walifanya dhambi walipomuuza mwenzao kwa jinsi ya kiroho walimuua kwa maana walitangaza mauti mpaka kwa baba yao na mama yao na wakalia msiba.
Kwa hiyo waliua na dhambi iliingia hapo na ile dhambi iliwatesa sana na ile dhambi ndio iliwafanya wakae pale mpaka wakawa watumwa baada Yusufu kufa. Sasa saa ya kutoka hawawezi kutoka mpaka wameshughulikia ile dhambi pale na kasome biblia yako katika agano La kale ilikuwa ni jino kwa jino kwa hiyo damu ikimwagika inasafishwa na Damu nyingine.
Sasa Mungu hakutaka kuua wazaliwa wao wa kwanza aliamua kumtoa kondoo kwa niaba yao ili kushughulika na dhambi ya kurithi na urithi mbaya unaowatesa, kwa hiyo hawawezi kutoka bila sheria kwa hiyo lazima atumie sheria kabla hajakuonesha haki yako wakati huu lazima ashughulike na kinachokukwamisha wakati huu usipate haki yako.
Kwa hiyo haijalishi dhambi zimetangulia miaka 400, zinaweza shikilia kizazi miaka na miaka kama hujui namna ya kutoka. Nimekueleza kitu cha namna hii ili ujue kuwa Musa alitangaza kwamba kila familia itafute kila mwanakondoo wamachinje na wapake ila Damu kwenye miimo ya malango na kizingiti cha juu.
Sasa yale maneno yalikuwa yanamhusu na yeye pia kwa sababu alikuwa anatangaza kutoka wakati na yeye na mke wake wako Misri, kwa sababu hawawezi kutoka kwa sababu ni watumishi bali ni kwa sababu wameiheshimu Damu ya Pasaka. maana haiwezekani waihubiri Damu ya Pasaka alafu wao wanafikiri watatoka kwa mkakati mwingine.
Sasa huwezi kuhubiri mkakati wa kutoka kwa kutumia Damu na wewe ukasema aaa mimi ni mtumishi wa Mungu nitatoka kwa mkakati mwingine. Hakuna njia ya staili hiyo, kwa hiyo Musa alikuwa anawaambia kama kungekuwa na simu kama leo mimi nafikiri angezima maana wengine wangekuwa wanampigia ili kumuuliza kuwa ivi ulisema kuwa tunamchinja saa ngapi, na wengine wangesema ivi unasema anaefanya kazi ya kuchinja ni baba au mama. Tunapochinja je tunafanya sala yoyote au je watoto wa kike na wakiume wanaruhusiwa kwenda kumwaga Damu? mara simu nyingine inapigwa ili kuuliza hiki na kile.
Ni rahisi sana kusoma yale maneno na ukafikiri kilikuwa ni kitu chepesi kwa hiyo nae Musa kama anataka kutoka hana namna nyingine ambavyo akiweka ile damu na akatoka ina maana atapigwa yeye mwenyewe kwa sababu kavunja sheria na familia yake haitapona. Haponi kwa sababu yeye ni mtumishi wa Mungu bali ni kwa sababu ametumia maandiko yale yale aliyoambiwa ahubiri na ile ile Damu ndio atakayoitumia.
Kwani hatuhubiri kwa sababu hatuna shida au sisi ni wasafi kuliko wengine mtu asikudanganye kuwa kwa sababu eti ni mhubiri yeye hana shida, maana hamna mtu anapeleka application kwa Mungu kuwa tufanye kazi anachagua kwa neema yake, kwa kusudi lake na kutaka kwake si kwa sababu ni wasafi ila ni kwa sababu anataka. kasome biblia yako inasema aliwachagua wanafunzi wake kama alivyotaka mwenyewe
Ndio maana hutaenda mbinguni kwa sababu ya cheti cha utumishi Lazima Damu ya Yesu ifanye kazi. Kama unafikrii natania kasome biblia yako maana Yesu atasema haloo ondoka hapa wewe utendae maovu maana sikuji wewe. utasema pole pole Yesu mbona nilikuwa natoa unabii na nilikuwa nakemea pepo na linatoka.
Sasa kwanini unasema hunijui wakati yote ulikuwa unatenda, atasema ni kwa sababu ya neno langu na jina langu ndio nilikuwa natenda. Ndio maana ninakuambia imani yako itakusaidia wakati Musa wako nae yupo nyumbani kwake na anaomba na kutoka nae kivyake.
Saa hiyo sio wakati tena wa kumpigia simu kusema naomba unisaidie wakati na atawajibu kuwa maneno yale niliyowambia yamenifunga na mimi na sina namna ya kutoka.
Ngoja nikupe mfano huu;
*USHUHUDA*
```Kuna dada mmoja alikaa kwa mume wake na alikuwa anapata mimba na zinaharibika na ziliharibika karibu mimba kama sita hivi. tulikuwa mahali fulani kwenye nyumba fulani alitusikia pale na kesho yake ofisini tuliletewa barua 7 full scale,anajieleza. Akajieleza matatizo yake na akasema kama Mungu akiwapa kibali mnisaidie. Basi tulijadaliana na mke wangu baada ya kuomba na tukamtafuta akaja tuliongea na tukamtia moyo vizuri kabisa na baada ya muda alipata ujauzito na tulimpa na mistari. Baada ya miezi miwili akaja tena ofisini akaniambia kuwa mimba imetoka. nikamuuliza swali kwanini umetoa mimba? akasema nimeenda chooni imetoka yenyewe. nikajua hakuelewa swali langu.
Nikamuuliza umewahi kuona maiti inapata mimba? akasema hapana nikamuuliza tena je, kinachopata mimba ni mwili au roho?. nikamuuliza kuwa kama mwili usipokuwa na roho haupati mimba je kinachopata mimba ni roho au mwili.? akanitazama akasema ni roho.
nikamwambia mwili kazi yake ni kutengeneza mwili, kwa hiyo nikamwambia kama roho yako ndio inayopokea ujauzito na kukabidhi kwa mwili ili kutengeneza mwili.
sasa nikamuambia kwa hiyo mwenye mamlaka ya mwisho ya kupata mimba sio mwili ni roho. kwa hiyo nikampeleka kwenye maandiko. na kumsemesha mtoto kukaa tumboni kuwa haruhusiwi kutoka kabla ya miezi tisa. Na nilimpa na mistari na nilimfundisha tena kitu cha kufanya.
Baada ya muda tena alipata mimba na tukasema tutazidi kukuombea. sasa baada ya miezi miwili akaanza kuona Dalili za kutoka kwa mimba tena, na alitutafuta ofisini na kila mahali na alitukosa.(Tulikuwa eneo lile lile pale pale mjini)
Alitutafuta kila mahali hakutupata, basi akarudi nyumbani kwake amenyong’onyea. sasa alipofika kwake Roho Mtakatifu alimkumbusha ile mistari niliyompa. na yule mama akaanza kufuatilia ile mistari tuliyompa wakati ule na ghafla ile haja ya kuwa na imani yake peke yake ikaongezeka. Sasa unapozungukwa na watu wanao kusaidia kukuombea na itafika kipindi, unapotafuta mpenyo na sisemi kuombewa ni vibaya. sasa itafika mahali unataka kupiga simu na kwa kuwa unakuwa kwenye mahangaiko unaweza kuta hata simu hukuchaji vizuri na inazima.``` Hapo unakuwa huna mtu tena wa kukusaidia na *ndio maana kuwa na imani yako mwenyewe ni muhimu.*
Kwa sababu hiyo Mungu alimwambia Musa kuwa, lazima kila mtu aende zizini, ndio maana nasema ukisoma Waebrania 11 utafikiri ni Musa aliwafanyia ila ukisoma katika Kutoka unaona jinsi ambavyo Mungu alikuwa anasisitiza umuhimu wa kuwa na imani binafsi juu ya Damu ili kila mmoja kule ndani aweze kufanya peke yake. Maana kuna kipindi unaweza kuwa na akina Musa wengi sasa si vibaya maana watakusaidia kuomba. Ila kuna kipindi, imani yako inakuwa chini kiasi ambacho huna hata msaada tena na hapo ndipo umuhimu wa kuwa na imani binafsi unaongezeka. Biblia inasema nitafuatia mfalme akiwa amechoka maana ndio saa ambayo unakuwa huwezi hata kufanya lolote. na *ndio maana ni muhimu kuwa na imani yako hata kama ni kidogo*.
*3. IMANI YAKO HIYO ITAKUSAIDIA WEWE NA FAMILIA YAKO WAKATI WATU WANAOKUHUSU WAMEAMUA KUTOKUAMINI MANENO YA MUSA JUU YA DAMU*
Wana wa Israel najua katikati yao walikuwepo wabishi yaani watu ambao hawakuamini. maana kuna namna ubishano ulikuwepo kwa mfano Musa alipooa mwanamke Mkushi kuna wengine walibisha, kuwa haiwezekani Mungu aseme na Musa peke yake. na najua pia kuna wengine walikuwa hawaoni kwao kwa sababu kwao kulikuwa na mwanga ila kwa wengine ilikuwa giza. Musa na Haruni kila walichoambiwa na Mungu hawakubisha maana waliona Mungu akitenda.
Naamini walikuwepo waliosema haiwezekani Bwana hii damu ya kondoo ndio tuitumie hivyo, labda wangetuambia kuwa tupake juu ya wazaliwa wa kwanza ni sawa ila, hii ya kutuambia hii *DAMU YA KONDOO NDIO IWE DAMU YA PASAKA*, alafu tupake kwenye milango na kizingiti cha juu wazaliwa wa kwanza watapona.
Lazima kuna watu walisema sisi ni uzao wa Ibrahimu hatuwezi kukutana na shida ya namna hii na kumbuka pia kuna wapendwa nao wanasema aaah mimi nimeokoka siwezi kutana na shida ya namna hii, na wanaacha DAMU pembeni. Kumbuka hawa Wayahudi kuna siku moja walibishana na Yesu na kusema sisi ni uzao wa Ibrahimu hatujawahi kuwa watumwa wa dhambi hata siku moja walikuwa wabishi na ndio maana Mungu aliwaita wenye shingo ngumu. kwa hiyo imani yako ni muhimu sana ili kuweza kushinda ubishi wa namna hii.
Ni sawa sawa na watu ambao wanabisha kuokoka na siku wakikutana na Yesu ndipo watakukumbuka au wakienda ule upande wa Pili ambao alienda yule tajiri wakati wa Yesu alipotoa mfano wa Lazaro ndipo watakumbuka umuhimu wa Mpendwa wao aliyekuwa anawashuhudia habari za Mungu.
*4. IMANI YAKO HIYO ITAKUSAIDIA WEWE NA FAMILIA YAKO WAKATI MNAEMTEGEMEA KIIMANI ANAPOKUWA MZITO KUWAONGOZA KATIKA NJIA YA DAMU YA YESU*
Musa alimtegemea Haruni ila ndiye aliye waongoza watu kuabudu ndama. Ile kwamba wote mmeamka mna Yesu haina maana ikifika jioni wote mna Yesu. huwezi jua kitu kinachopita hapo mchana.
Na unakuta ni mtu mlikuwa mnaemtegemea sana kiimani na mnamkuta anakuja na ndama nyumbani mnamuuliza je huyu wa kuchinja au, anasema hapana ni wa kuabudu mnamuuliza imetoka wapi anasema mafunuo haya Bwana nimeonana na Mungu kwenye maombi.[ndio maana ni hatari kuwa na maombi bila neno, maombi yanaendana na neno].
Unaweza kuta mtu anasema ili akusaidie anasema leta sadaka kwanza, maana sadaka haiwezi kununua kitu kutoka katika kitu cha msalabani. Najua sehemu ya sadaka na umuhimu wa sadaka na hutoi sadaka kwa sheria bali unatoa kwa imani. kwa hiyo mtu asikulazimishe kutoa sadaka bali toa kwa imani.
Je kama mtu mnayemtegemea hayupo mtafanyaje? ndio maana lazima awepo mwingine, na ndio maana neno la Mungu halifungwi yaani mkimuua Yakobo, jua kuwa Petro yuko. Na mkimuua Petro mwingine atasimama.
Kwa hiyo jenga imani yako ndani ya damu ya Yesu maana kila aliyeokoka ana kazi na anaweza tumia Damu ya Yesu. Biblia inasema iweni hodari katika Bwana katika nguvu zake. Kwa hiyo iweni hodari na vaeni silaha zote. Huwezi kuwa Hodari kama hufanyii mazoezi ulichosoma
Ndio kama Kocha wa mpira anataka mtu hata kama ni mzuri sana anaweza kupiga chenga sana na kucheza vizuri, lazima afanye mazoezi ili ajue namna ya kucheza kiteam na kuwapasia wenzake ili kila mtu aweze kuwa na uwezo wa kufunga goli na adui ashindwe amkabe yupi. Maana hata goalkeeper anafundishwa namna ya kufuga goli.
Kwa hiyo chukua ile *Waebrania 9:16-17*, maana palipo na agano la urithi lazima kuwepo na mauti na wewe chukua mauti ya Yesu maana inapangua mauti zingine. Kwa hiyo chukua haya maneno tafakari na chukua hili maana hata mimi kabla sijaleta hapa lazima nione kinafanya kazi.
Huwezi kushugulikia masuala ya urithi mbaya kama hujaokoka maana Damu ya Yesu ni damu ya agano na sio kila mtu na unaingia kwenye agano kwa kuokoka ili uwe na haki. Hawezi kukuonesha haki yake kama Damu haijamwagika mahali.
ooh.. Funika macho yako… Kama hujaokoka hakikisha unaokoka na kumpokea Yesu awe Bwana wa maisha yako..
🎶🎶wimbo wa _*Ni Salama Roho moyoni Mwangu.🎶*_🎶
Baada ya hapo bonyeza link pale juu kusikiliza maombi ya kuokoka na baraka. Pia kuna namba za sadaka ziko pale kama utasukumwa na Roho Mtakatifu kutoa au kumshukuru Mungu kwa neema hii ya kupata masomo haya kwa siku zote nane.
*Tuonane tena semina ijayo Njombe kuanzia Alhamisi 19-22 OCT 2017*. *Ubarikiwe sana na Yesu 🙏🙏🙏*
Huduma Ya Mana Tanzania na Mwalimu Christopher Mwakasege
mwakasege.org

No comments:

Post a Comment

Urithi wa watumishi wa Mungu

URITHI WA WATUMISHI WA MUNGU. ------------------------------------------------------------ Hii wengi hawafahamu lakini leo fahamu japo k...